Rais William Ruto amewataka Wakenya kutoruhusu mtu yeyote kukatiza ndoto zao za kumiliki nyumba.
Alisema Wakenya sasa wanaweza kuchangia kwa hiari kumiliki nyumba bora, kutokana na mpango wa nyumba za bei nafuu ambao ni sera ya serikali.
“Tutawasilisha maelfu ya nyumba katika maeneo mbalimbali chini ya Mpango wa Nyumba za Bei nafuu wa Nyandarua na kubuni nafasi za kazi kwa maelfu ya vijana wetu katika kaunti hii,” aliwaelezea wakazi.
Kiongozi wa nchi aliwataka Wakenya kupiga *832# kwenye simu zao na kujisajili kwenye tovuti ya Boma Yangu. Baada ya kujiandikisha, mwanachama hupewa nambari ya kipekee ya utambulisho, ambayo huitumia kuangalia na kuhitimu kumiliki nyumba anazopenda.
Alisema Wakenya wa tabaka mbalimbali wanastahiki mradi huo bora tu wachangie na wanaweza kulipa kila siku au kwa raha zao.
Akizungumza wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa mpango wa nyumba za bei nafuu wa Ol Kalou katika Kaunti ya Nyandarua, Rais Ruto alisema asilimia 20 ya nyumba hizo – nyumba za kijamii – zitatengwa kwa watu wa boda boda na mama mboga.
“Ili kulipia nyumba hizi, mtu atahitajika kulipa rehani ya kati ya shilingi 3,200 na 6,000 kwa mwezi kwa riba ya asilimia 3 kwa miaka 15 kutegemea nyumba,” alisema Rais Ruto.
Alisema amana ya chini ya shilingi 80,000 itahitajika kutoka kwa wafanyabiashara wa boda boda na mama mboga ili kumiliki nyumba hizo.

Hii inamaanisha kuwa nyumba za jamii zitagharimu kima cha chini cha shilingi 800,000.
“Ikiwa boda boda na mama mboga wataweka akiba ya shilingi 150 kila siku, wataongeza amana inayohitajika katika muda wa miezi 18. Hii itatosha kuanza mchakato wa kumiliki nyumba nzuri,” Rais alisema.
Aina ya pili ya nyumba za bei nafuu itagharimu kati ya shilingi 5,000 na 15,000 kwa mwezi, kutegemea nyumba ya chaguo, kwa riba ya asilimia sita.
Kwa aina ya bei ya soko ya nyumba, vitengo vitahitaji malipo ya kila mwezi ya shilingi 25,000 na zaidi kwa riba ya asilimia 9.
“Tumepunguza kwa kiasi kikubwa riba ya mpango wa nyumba za bei nafuu kutoka ilivyo sokoni,” aliongeza.
Katika ziara yake ya siku moja katika Kaunti ya Nyandarua, Rais aliandamana na Naibu Rais Rigathi Gachagua, Mawaziri Kipchumba Murkomen, Alice Wahome na Zachary Njeru, Gavana Kìariì Badilisha, wabunge na viongozi wengine wa eneo hilo.