Mshukiwa wa wizi wa watoto akamatwa

Tom Mathinji
1 Min Read
Mshukiwa wa wizi wa watoto Mary Akinyi Mulamula.

Maafisa wa polisi wa idara ya kukabiliana na makosa ya jinai DCI, wamemkamata mshukiwa wa wizi wa watoto, huku wakiwaokoa watoto wawili ambao walikuwa wametekwa nyara.

Mary Akinyi Mulamula, ambaye amekuwa akikwepa mtego ya maafisa hao wa polisi, hatimaye alitiwa nguvuni, na anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Kabete, Jijini Nairobi.

Mshukiwa huyo alikamatwa baada ya kuwasilishwa kwa ripoti kuhusu kuibiwa kwa mtoto kutoka nyumbani kwao katika kijiji cha Virhembe kaunti ya Kakamega mnamo Juni 6, 2024.

Kulingana na idara ya DCI kupitia mtandao wa X, mshukiwa huyo alichukua mtoto huyo huku akisingizia alikuwa akimpeleka kusajiliwa kwa mpango wa ufadhili wa shilingi 9,000 kila mwezi.

Hata hivyo, mshukiwa huyo alitoweka na mtoto huyo na kuwaacha familia ya mtoto huyo ikihangaika.

Kufuatia uchunguzi wa kina, maafisa hao wa DCI walimuokoa mtoto huyo na kumtia nguvuni mshukiwa huyo, pamoja na kumuokoa mwathiriwa mwingine. Mshukiwa huyo anazuiliwa na polisi.

TAGGED:
Share This Article