Maafisa wa polisi wamemkamata mshukiwa wa wizi wa simu za mkononi, anayedaiwa kuwa huwa anapokea rununu zilizoibwa katika eneo la Kisauni na viunga vyake.
Ndaziziye Augustin Umurundi, ambaye ni raia wa Rwanda, alikamatwa nyumbani kwake baada ya maafisa wa polisi kupokea habari za ujasusi.
Baada ya msako katika nyumba yake, maafisa hao walipata mamia ya simu za mkononi, pamoja na vifaa vingine vya kielektroniki vinavyoaminika kuwa vya wizi.
Miongoni mwa simu zilizonaswa ni pamoja na rununu aina ya Tecno Spark KJ5, iliyoibwa kutoka kwa Stephen Omondi katika enel la Tudor Novemba 5, 2024, Tecno Spark K15K iliyoibwa kutoka kwa Aberdeen Jafferji katika daraja la Nyali Novemba 1, 2024, na Samsung Galaxy A15, iliyoibwa kutoka kwa Charles Ogeyo katika eneo la Mishomoroni Novembea 4, 2024.
Kwa sasa maafisa wa polisi wanawatafuta wenye simu zilizosalia, huku mshukiwa akizuiliwa katika korokoro za polisi akisubiri kufikishwa mahakamani.