Mshukiwa anayedaiwa kumwibia na kumbaka mwanamke mmoja majuma matatu yaliyopita amekamatwa.
James Mwangi Wanjahi mwenye umri wa miaka 39, ambaye polisi wanasema alitoweka tangu tarehe 17 mwezi Februari mwaka huu baada ya kutenda kosa hilo, alikamatwa na maafisa wa upelelezi.
Mshukiwa huyo alifurushwa kutoka mafichoni katika eneo la Kabete, ambapo simu iliyoibiwa kutoka kwa mwathiriwa ilipatikana.
Kwa mujibu wa ripoti ya polisi, mshukiwa huyo alimlaghai mwathiriwa huyo mwenye umri wa miaka 40 katika mpango wa biashara kabla ya kumtendea unyama huo.
Inadaiwa kuwa mwathiriwa huyo aliripoti kisa hicho katika kituo cha polisi cha Kikopey huko Gilgil kwamba mwanamume mmoja aliyejifanya mteja anayemfahamu, alipendekeza wakutane katikati mwa jiji la Nairobi kwa mazungumuzo kuhusu biashara lakini akabadili nia alipopanda gari lake.
Wakati wa tukio hilo, mlalamishi aliibiwa pesa taslimu shilingi 17,000 na kisha kubakwa. Mshukiwa huyo anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Gilgil akisubiri kufikishwa mahakamani.