Mshukiwa wa ulanguzi wa bangi akamatwa Nairobi

Tom Mathinji
1 Min Read
Mshukiwa wa ulanguzi wa bangi akamatwa Nairobi.

Maafisa wa polisi wamemkamata mshukiwa wa ulanguzi wa bangi aliyetoroka mtego wa polisi Julai 10, 2024 katika kaunti ya Kisii.

Mshukiwa huyo alitoroka na kuacha gari aina ya Nissan X-Trail lenye nambari za usajili KDP 353U, lililopatikana na bangi ndani yake.

Walipokuwa wakishika doria katika barabara kuu ya Kisii-Migori, maafisa wa polisi walisimamisha gari hilo lililokuwa likiendeshwa kwa kasi kuelekea upande wa Kisii.  Dereva alikataa kusimama na kusababisha maafisa hao kulifuata.

Gari hilo lilipoteza mwelekeo na kuingia ndani ya shimo, huku watu watatu waliokuwemo wakitoroka kwa miguu na kuliacha.

Baada ya kupekua gari hilo, maafisa hao walipata kilo 112.8 za bangi ya thamani ya shilingi 3,384,000.

Hata hivyo, baada ya kuanzisha msako dhidi ya walanguzi hao, maafisa hao walifanikiwa kumtia nguvuni mshukiwa mkuu Samuel Omondi mwenye umri wa miaka 36.

Omondi alipatikana katika maficho yake mtaani Kibra jijini Nairobi.

Omondi alifikishwa mahakamani, huku msako dhidi ya wenzake ukiendelea.

Website |  + posts
TAGGED:
Share This Article