Mshukiwa wa misururu ya mauaji kaunti ya Narok afikishwa mahakamani

Tom Mathinji
1 Min Read
Mshukiwa wa misururu ya mauaji Kaunti ya Narok afikishwa mahakamani.

Mshukiwa ambaye amehusishwa na misururu ya mauaji kaunti ya Narok, alifunguliwa mashtaka katika mahakama moja ya Narok.

Musa Ole Sopia almaarufu Ololunga, anatuhumiwa kuhusika katika visa kadhaa vya mauaji mjini Narok mwezi Septemba, ambapo takriban watu 10 walifariki kupitia hali tatanishi.

Mshukiwa huyo alitiwa nguvuni baada ya kunakiliwa na kamera fiche za CCTV akijihusisha na wizi na pia mauaji ya bawabu raia wa Congo mwenye umri wa miaka 55 katika kituo cha kibiashara cha Ololulunga.

Mshukiwa huyo alifikishwa mbele ya hakimu mkaazi wa Narok Daniel Ngayo, aliyeagiza afanyiwe uchunguzi wa kiakili katika kituo cha afya cha serikali kabla ya kushtakiwa.

Wakati huo huo, hakimu huyo aliagiza kuwa mshukiwa huyo azuiliwe katiku gereza la Narok hadi Novemba 26, 2024 wakati ambapo atafikishwa tena mahakamani.

Kamanda wa polisi wa kaunti ya Narok Riko Ngare, alisema kuna ushahidi wa kutosha kumhusisha mshukiwa huyo na mauaji hayo.

Share This Article