Maafisa wa polisi wamemtia nguvuni Paul Odhiambo Owuodho, almaarufu Fazul Mohammed, kwa madai ya kumpiga risasi Abdirahim Abdullahi katika mtaa wa Eastleigh juma lililopita.
Mshukiwa huyo mwenye umri wa miaka 27, pia amehusishwa na mauaji ya afisa wa upelelezi wa makosa ya jinai (DCI) katika mtaa wa Mihango Jijini Nairobi, mwaka uliopita.
Odhiambo alitiwa nguvuni, baada ya maafisa wa DCI kufanya operesheni katika kaunti ya Kiambu.
Kulingana na maafisa wa polisi, Odhiambo alikuwa anatafutwa kuhusiana na mauaji ya Abdullahi Novemba 9,2024 yaliyotekelezwa kwenye jengo la DD Plaza, mtaani.
Fauka ya hayo, mshukiwa huyo pia alihusishwa na mauaji ya afisa wa polisi konstebo David Mayaka.
Mayaka alipigwa risasi na majambazi waliokuwa kwa pikipiki Agosti 23, 2023 mtaani Mihang’o aliposimama kurekebisha gurudumu la gari lake.
Mshukiwa huyo anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Shauri Moyo, huku uchunguzi ukiendelea.