Mahakama ya Kabarnet imemhukumu mwanamume kifungo cha miaka 30 gerezani kwa kuwadhulumu kimapenzi watoto wawili, mmoja mwenye umri wa miaka minne na mwingine mitatu.
Makosa hayo yanadaiwa kutekelezwa Agosti 12,2024 katika kata ya Ilchamus, kaunti ndogo ya Baringo kusini kaunti ya Baringo.
Upande wa mashtaka ukiongozwa na Claire Kosgei na Collins Ogutu, uliwasilisha mashahidi tisa, waliotoa ushahidi wao kuunga mkono mashtaka dhidi ya mshukiwa huyo.
Mshukiwa huyo alishtakiwa kwa makosa mawili ya dhuluma za kimapenzi chini ya sehemu ya 8(1) ya sheria za makosa ya dhuluma za kimapenzi.
Aidha mshukiwa huyo alikabiliwa na makosa mengine mawili tofauti ya kushiriki mapenzi na watoto chini ya sehemu ya 11(1) ya sheria za dhuluma za kimapenzi.
Akitoa hukumu hiyo, Jaji Koskey alibainisha kuwa upande wa mashtaka ulidhibitisha bila hofu mshukiwa huyo alikuwa na hatia.