Mshukiwa wa biashara haramu ya dhahabu akamatwa

Tom Mathinji
2 Min Read
Jonathan Okoth Opande almaarufu Okoth Magawi

Jonathan Okoth Opande almaarufu Okoth Magawi, ametiwa nguvuni kwa madai ya kuwalaghai raia wawili wa Thailand shilingi milioni 13, kupitia biashara haramu ya dhahabu.

Kulingana na taarifa kutoka idara ya upepelezi wa jinai DCI, Opande ambaye anafahamika pia kama kiongozi, aliondolewa ndani ya ndege ya shirika la Kenya Airways iliyokuwa ikielekea Kisumu Ijumaa alasiri, na maafisa wa upelelezi waliofahamishwa kuhusu ratiba yake ya safari.

“Baada ya kuepuka mitego kadhaa ya polisi miezi kadhaa iliyopita, mmoja wa walaghai wa dhahabu bandia Jonathan Okoth Opande almaarufu Okoth Magawi, ametiwa nguvuni,” ilisema taarifa ya DCI.

Mshukiwa huyo ambaye aliwania kiti cha ubunge cha Nyakach bila kufanikiwa katika uchaguzi mkuu uliopita, amekuwa akikwepa mtego wa maafisa wa upelelezi, huku akitafutwa kuhusiana na kesi ambapo aliwalaghai raia wawili wa Thailand shilingi milioni 13.

Kulingana na taarifa ya polisi iliyoandikishwa katika ubalozi wa Thailand hapa nchini mwezi Aprili mwaka huu na Kitvisit Songsri na Nutsaphol Songsri, mshukiwa huyo akijidai kuwa afisa mkuu mtendaji wa kampuni ya Blu Afrique, alipokea fedha hizo kwa kisingizio kuwa atawasambazia dhahabu ambayo kiwango chake hakikubainika.

DCI ilisema raia hao wawili wa kigeni walisafiri humu nchini tarehe 17 mwezi Aprili kukamilisha biashara hiyo, kabla ya kugundua baadaye kuwa walihadaiwa katika biashara bandia ya dhahabu.

Msako uliofanywa na maafisa wa polisi katika afisi ya mshukiwa iliyoko mtaani Lavington, ulisababisha kupatikana kwa mihuri ya halmashauri ya ukusanyaji ushuru nchini KRA, mashini za kupima uzani na koti zilizo na nembo za wizara ya madini.

Share This Article