Mshukiwa mkuu wa mauaji ya maafisa wawili wa Polisi akamatwa 

Tom Mathinji
1 Min Read

Mshukiwa mkuu wa mauaji ya maafisa wawili wa polisi waliokuwa wameenda kudai deni lao Trans Mara kaunti ya Narok, amekamatwa. 

Maafisa wa kitengo cha Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), walimkamata mshukiwa huyo aliyetambuliwa kwa jina Pius Lemiso Ndiwa, katika mbuga ya wanyama ya Maasai Mara akiwa mafichoni.

Ndiwa alinaswa usiku wa Jumanne baada ya kuwakwepa polisi kwa siku kadhaa. Mshukiwa huyo ambaye pia ni afisa wa polisi anakabiliwa na kosa la kupanga mauaji ya wenzake wawili Juma lililopita.

Wawili hao waliuawa katika kijiji cha Olemismis baada ya kuitwa na Ndiwa kuja kusuluhisha deni la chama cha ushirika.

Polisi waliouawa walitambuliwa kuwa Inspekta Patrick Mukunyi Kuya na Sajini Mkuu Daniel Nairimo.

Wawili hao walifunga safari kutoka Nairobi siku ya Jumatano iliyopita wakielekea Trans Mara kusuluhisha deni la mkopo ambalo Ndiwa alikuwa amekataa kulipa.

Walipofika nyumbani kwa Ndiwa, walikabiliwa na vijana wawili wa kiume kwa panga na mishale na kuuawa papo hapo.

Ndiwa alikuwa ameambia familia yake kuwa wawili hao walikuwa majambazi.

Ndiwa alipelekwa katika kituo cha polisi cha Kilgoris kabla ya kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya mauaji.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Share This Article