Mshukiwa azuiliwa, bunduki iliyoibwa Kirinyaga yapatikana

Martin Mwanje
1 Min Read

Makachero wa idara ya upelezi wa jinai, DCI wamepata bunduki aina ya AK47 ambayo ilikuwa imeibwa kutoka kituo cha polisi cha  Kabonge katika kaunti ya Kirinyaga Februari 2, 2024. 

DCI inasema mwanamume mwenye umri wa miaka 25 amekamatwa kuhusiana na wizi huo.

“Mshukiwa, Kennedy Mwangi Wangeci anayetokea eneo la Mugure huko Ndia alifumaniwa na makachero waliokuwa na taarifa za kijasusi kabla ya bunduki hiyo na risasi 18 kupatikana zikiwa zimezikwa katika shimo la kina kifupi nje ya nyumba yake,” ilisema DCI katika taarifa.

Afisa wa polisi aliyemiliki bunduki hiyo ya AK47 na mwingine aliyemiliki bunduki aina ya G3 ambayo pia iliibwa kwa sasa wanachunguzwa.

Msako wa kutafuta bunduki aina ya G3 umeshika kasi.

Mshukiwa anahojiwa ili kutoa maelezo zaidi kuhusu namna alivyopata bunduki hiyo.

Share This Article