Maafisa wa polisi Jijini Nairobi, wanamzuilia mshukiwa kuhusiana na kupatikana kwa bidhaa za mapishi zinazoshukiwa kuwa za wizi.
Kulingana na huduma ya taifa ya polisi, shehena iliyokuwa na bidhaa hizo, iliibwa ikiwa safarini kutoka bandari ya Mombasa kuelekea Malindi.
Maafisa wa polisi kutoka Nairobi na Mombasa waliofanya operesheni ya kusaka bidhaa hizo, walimnasa mshukiwa huyo katika mtaa wa Saika Jijini Nairobi.
Shehena hiyo ilikuwa na bidhaa za thamani ya shilingi milioni kumi iliyoibwa baada ya dereva wa lori lililokuwa likisafirisha bidhaa hizo kuzielekeza kwingine akisingizia kuwa lori hilo lilikumbwa na hitilafu la kiufundi katika eneo la Kikambala, katika barabara kuu ya Mombasa-Malindi, hatua iliyosababisha mwenye mizigo hiyo kupiga ripoti kwa polisi.
Mshukiwa mmoja Francis Victor Karua Gathii, alitiwa nguvuni huku akiwasaidi maafisa wa polisi kwa uchunguzi.