Mshukiwa akamatwa na pembe za ndovu Kibwezi

Marion Bosire
1 Min Read

Kundi la maafisa wa vitengo mbali mbali vya usalama nchini wakiwemo wa upelelezi wa jinai DCI wanaohusika na makosa sugu na wa huduma kwa wanyamapori KWS wamekamata mshukiwa aliyekuwa na vipande vya pembe za ndovu huko Kambu, kaunti ndogo ya Kibwezi kaunti ya Makueni.

Katika hatua hiyo kubwa kwenye vita dhidi ya uwindaji haramu Sila Maweu wa umri wa miaka 57 na wenzake watatu waliotoroka walipatikana na kilo 84 za vipande vya pembe za ndovu.

Polisi waliokuwa wamepashwa habari na wananchi kuhusu washukiwa hao waliwavamia watatu wakatoroka Maweu akabaki akiwa na ushahidi wa pembe hizo.

Alifikishwa katika mahakama ya uwanja wa kimataifa wa Jomo Kenyatta JKIA ambapo alikubali mashtaka dhidi yake. Kesi yake itatajwa Agosti 26, 2024.

Huku washukiwa waliotoroka wakisakwa, maafisa wa usalama wameapa kutumia kila mbinu na raslimali hadi wakamatwe na kushtakiwa.

Wanyamapori fulani wako katika hatari ya kuangamizwa kabisa kwani wawindaji haramu wanawalenga kwa ajili ya pembe zao.

Biashara ya sehemu za miili ya wanyamapori imepigwa marufuku nchini kama hatua ya kulinda wanyama hao lakini uwindaji haramu bado ni tatizo nchini Kenya.

Share This Article