Mshauri wa Rais kuhusu Haki za Wanawake Harriette Chiggai sasa anataka mauaji ya wanawake kuchukuliwa kama suala nyeti la kitaifa.
Amesema idadi ya wanawake wanaouawa nchini inatia hofu.
Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI imesema wanawake wapatao 97 wameuawa katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita.
Chiggai amesema mwenendo wa mauaji ya wanawake kwa sasa unaashiria mwanamke mmoja anauawa kila siku na kutaka serikali kuwachukulia wahusika hatua kali.
Aliyasema hayo alipoandaa mkutano wa viongozi wanawake kabla ya uzinduzi wa mpango wa makazi salama, maeneo salama kwa wanawake mwezi Disemba mwaka huu.
Matamshi yake yanakuja siku chache baada ya Rais William Ruto kuiagiza DCI na vyombo vingine vya dola kufanya uchunguzi wa kina na kuwachukulia wale wote wanaohusika katika mauaji ya wanawake hatua kali.
Jaji Mkuu Martha Koome na Chama cha Mawakili Wanawake, FIDA ni miongoni mwa wale ambao wamepaza sauti zao wakitaka hatua kali kuchukuliwa kwa wahusika wa mauaji ya wanawake.