Msanii William Getumbe akamatwa

Tom Mathinji
1 Min Read
Msanii William Getumbe.

Bodi ya uorodheshaji filamu nchini, KFCB imesema kuwa mwanamuziki wa nyimbo za injili William Getumbe amekamatwa baada ya wimbo wake mmoja kuhusishwa na ukosefu wa maadili.

Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa bodi hiyo Nelly Muluka amesema msanii huyo alitiwa nguvuni baada ya kukamilika kwa makataa ya siku saba aliyopewa kuondoa wimbo huo mitandaoni.

“Bodi ya uorodheshaji filamu nchini, kupitia tawi lake la eneo la North Rift, mjini Eldoret na kwa usaidizi wa maafisa wa polisi kutoka kituo cha polisi cha Kapsoya, walimkamata na kumzuilia msanii William Getumbe, baada ya kukiuka sehemu ya 222 ya sheria za Kenya,” alisema Muluka kupitia kwa taarifa.

Wimbo wa Getumbe “Yesu Ninyandue”, uliibua hisia mseto kutoka pembe zote za nchi.

Kulingana na Muluka, Getumbe atakabiliwa na mashtaka matatu, yakiwemo kuchukua filamu bila leseni inayokiuka ibara ya pili kifungu cha nne sehemu ya 222 ya katiba ya Kenya.

Vile vile msanii huyo atashtakiwa kwa kusambaza na kuionyesha filamu na wimbo ambao uakiuka ibara ya tatu, kifungu cha 12 sehemu ya 222 ya katiba.

Juma lililopita, Getumbe na msanii Chris Embarambamba, waliagizwa kuondoa nyimbo zao katika mitandao yote kwa kukiuka katiba.

Share This Article