Msako dhidi ya uunganishaji maji haramu Mathioya wapamba moto

Martin Mwanje
1 Min Read

Kampuni ya usambazaji maji ya Gatamathi katika eneo bunge la Mathioya, kaunti ya Murang’a inakadiria hasara ya milioni thelathini kutokana na wizi wa maji kupitia uunganishaji haramu.

Katika juhudi za kukabiliana na swala hilo, kampuni hiyo imeanzisha msako mkali katika maeneo ya usambazaji maji huku wakishirikiana na maafisa wa kitengo kinacholinda mito na chemchemi za maji, maarufu kama Water Police Unit.
Kupitia ushirikiano huo, wameweza kutia mbaroni na kuwafikisha mahakamani watu zaidi ya watano huku wengi wa waliopatikana na kosa la kujiunganishia maji wakitoweka manyumbani mwao.
Wasimamizi wa kampuni ya usambazaji maji ya Gatamathi, maafisa wa utawala na wale wa kitengo maalum cha kulinda mito na chemchemi za maji wamewataka wakazi kuwa wastaarabu na kususia shughuli haramu za kujiunganishia maji na vile vile kutaka wale waliojiunganishia maji kufika katika ofisi ya usambazaji maji ya Gatamathi ili kuwasiliana na maafisa jinsi watakavyosaidiwa na hivyo kuepuka kutozwa faini kali.
Share This Article