Msaidizi wa mahakama ya Mombasa akamatwa kwa madai ya mlungula

Martin Mwanje
1 Min Read
Ben Wambua Muthoka, anayetuhumiwa kwa kuitisha hongo

Msaidizi wa mahakama ya Mombasa amejipata matatani baada ya kukamatwa na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi, EACC kwa tuhuma za kuitisha rushwa.

Inadaiwa mshukiwa, Ben Wambua Muthoka, aliitisha hongo ya shilingi 10,000 kutoka kwa mlalamikaji ili kumsaidia kuficha au kushikilia faili ambapo mlalamikaji huyo anakabiliwa na mashtaka katika kesi inayoendelea ya uhalifu.

“Kitendo hicho kilikusudiwa kuchelewesha au kuhangaisha mchakato wa haki,” ilisema EACC kwenye taarifa.

Baada ya kupokea malalamishi ya uitishaji rushwa kutoka kwa mlalamikaji Machi 13, EACC ilianzisha uchunguzi wake uliobaini madai hayo ni ya kweli.

Ilifanya operesheni ambayo matokeo yake yalikuwa kukamatwa kwa mshukiwa wakati akipokea fedha hizo.

Baada ya kukamatwa, mshukiwa alipelekwa katika afisi ya EACC ya kanda ya eneo la Lower Coast ili kuandikisha taarifa na kisha kuzuiliwa usiku kucha katika kituo cha polisi cha Central.

Ameachiliwa kwa dhamana ya shilingi 20,000 akisubiri kukamilika kwa uchunguzi.

Share This Article