Mradi wa makazi ya gharama nafuu wa Meru 2 wafikia asilimia 16 na unatarajiwa kukamilika Januari 2026

Mhandisi Jesee alizungumza na wanahabari katika eneo la mradi huo huko Mwendatu, mjini Meru, ambapo alisema kuwa wameajiri wafanyakazi kutoka makundi mbali mbali, wengi wao wakiwa ni wa maeneo hayo.

Marion Bosire
2 Min Read

Mradi wa nyumba za gharama nafuu wa serikali ya kitaifa wa Meru 2 umefikia asilimia 16 ya ufanisi na wahandisi wanasema wanajibidiisha kukamilisha mradi huo kufikia Januari 2026.

Kwa mujibu wa mhandisi Jesee Rukunyi wa kampuni ya Agrobriq Investment Ltd ambaye anatekeleza ujenzi huo, jumba hilo lina jumla ya nyumba 220 na maduka ya kibiashara.

Mhandisi Jesee aliyezungumza na wanahabari katika eneo la mradi huo huko Mwendatu, mjini Meru, alisema kuwa wameajiri wafanyakazi kutoka makundi mbali mbali, wengi wao wakiwa ni wa maeneo hayo.

Alisema kwa sasa wanatumia wafanyakazi 88 na wanahusisha wanafunzi wa vyuo vya mafunzo ya kiufundi kama sehemu ya kujifunza kwa vitendo, ingawa alibaini kuwa idadi ya wafanyakazi inaweza kuongezeka kadri muda unavyosonga.

Msanifu majengo Bisher Fawaz ambaye anaongoza kundi la watekelezaji wa mradi huo wa Meru 2, alisema wanajenga nyumba za chumba kimoja, vyumba viwili na eneo la maduka pamoja na uwanja wa watoto kuchezea.

Alisema jumba hilo linaafiki viwango vya kimataifa ambapo wamiliki wa nyumba hawatakuwa na haja ya kutoka nje kununua bidhaa mbali mbali kwani kuna maduka humo.

Naibu Kamishna wa eneo la Imenti Kaskazini, Odilia Ndeti alisema mkataba wa mkandarasi unatekelezwa kama ilivyoainishwa katika nyaraka za mkataba.

Alisema wakazi wanaotaka kumiliki nyumba chini ya mradi wa nyumba za gharama nafuu wa serikali wameelekezwa ipasavyo kwa wizara ya nyumba kuhusu jinsi ya kupata nyumba baada ya mradi kukamilika na kutangazwa.

Odilia alishauri jamii ya maeneo hayo kununua nyumba zitakapotangazwa ili waweze kufaidika na mradi huu wa makazi ya gharama nafuu wa serikali.

Mmoja wa mafundi wa mradi huo kwa jina Nicholas Buudi Ibrahim alisema mradi huo umekuwa na manufaa makubwa kwake akiwa fundi mjenzi.

Alisema ameweza kutunza familia yake, kuweka chakula mezani na kulipa gharama nyingine za familia. Bundi aliomba serikali kuu kuendelea na miradi ya aina hii ili wananchi wa Kenya waweze kufaidika nayo.

Alitoa wito kwa vijana wanaolalamikia ukosefu wa ajira nchini, kujiingiza katika miradi kama hiyo ya serikali.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *