Katibu wa teknolojia ya mawasiliano na uchumi dijitali Mhandisi John Tanui amesema kwamba mpango mkuu wa Kenya wa kidijitali na mradi wa KDEAP vitaiweka Kenya mbele katka kanda hii katika masuala ya teknolojia.
Aliyasema hayo alipohudhuria warsha ya wadau wa mradi wa kuchapuza uchumi dijitali nchini yaani Kenya Digital Economy Acceleration Project -KDEAP katika hoteli ya Norfolk jijini Nairobi.
Mradi wa KDEAP, ambao unafadhiliwa na benki ya dunia kwa dola milioni 390, ni mpango ulioanzishwa na serikali ya Kenya kwa lengo la kuimarisha uchumi dijitali nchini.
Unaangazia upanuzi wa upatikanaji wa mtandao wenye kasi ya juu, kuimarisha uzuri na uwasilishaji wa elimu na huduma za serikali kwa kuwekeza katika majukwaa ya dijitali na huduma pamoja na kuandaa ujuzi wa kidijitali kwa vijana na hivyo kuboresha uwezo wao wa kushindana na wengine katika soko la ajira humu nchini na ughaibuni.
Katibu Tanui alisisitiza kwamba mpango huu ni muhimu katika kuinua Kenya kuwa kiongozi katika masuala ya dijitali katika kanda ya Afrika mashariki.