Serikali kuu imefufua matumaini ya kurejesha bwawa la Umaa katika kaunti ya Kitui huku mwanakandarasi akiwa amefika katika eneo hilo.
Mradi huo huo ulikwama zaidi ya miaka kumi iliyopita baada ya fedha zilizotengwa kwa ajili yake kutumiwa visivyo.
Serikali kuu inasemekana kutenga zaidi ya shilingi milioni 200 mwaka huu wa fedha kwa ajili ya kukamilisha bwawa hilo ambalo litagharimu walipa ushuru bilioni 1.9.
Simon Kimaru mwenyekiti wa shirika la kitaifa linalohusika na uhifadhi wa maji nchini alizuru eneo la mradi ambalo liko kilomita chache kutoka mjini Kitui ambapo alisema kwamba serikali imejitolea kukamilisha bwawa hilo katika muda wa miaka miwili.
Kimaru alisema pia kwamba wanafanya kila juhudi kuona kwamba Rais William Ruto anazindua upya ujenzi wa bwawa hilo kufikia mwezi ujao wa Machi.
Mbunge wa eneo hilo Daktari Makali Mulu alisema kwamba wakazi wa eneo hilo wanaridhika kuona mradi kama huo karibu nao hata ingawa awali walikuwa wamepoteza matumaini kufuatia kukwama.
Makali alielezea matumaini makubwa kwamba mradi huo utakamilishwa zamu hii, kwa sababu ujenzi wake unaungwa mkono na Rais aliye mamlakani.