Mr. Blue amiminia mkewe sifa

Marion Bosire
2 Min Read

Mr. Blue ambaye ni mwanamuziki wa mtindo wa Hip-Hop na Bongo Fleva kutoka nchini Tanzania amemmiminia sifa mke wake aitwaye Waheeda, akisimulia historia ya mapenzi yao ya zaidi ya miongo miwili na kubarikiwa na watoto watatu.

Blue ambaye jina lake halisi ni Khery Sameer Rajab, alisema hayo wakati akimtakia mke wake mema kwenye siku yake ya kuzaliwa. Alisimulia kwamba walikutana mwaka 2003 wakiwa bado wadogo, lakini mapenzi yao yalikuwa imara tangu mwanzo.

“Tulikutana mwaka 2003 tukiwa wote bado ni wadogo sana na tukapendana sana na mpaka leo hatujaacha kupendana” alisema Mr. Blue.

Msanii huyo aliendelea kuelezea anavyompenda mke wake na jinsi alivyo sehemu muhimu ya maisha yake. “Kiukweli nampenda sana huyu mwanamke na sidhani wala sijui kama kuna maisha mengine bila ya yeye” alisema.

Katika kuadhimisha siku ya kuzaliwa ya Waheeda, Mr. Blue aliomba mashabiki wake kushiriki shangwe hizo kwa kumtakia heri.

“Amezaliwa siku kama ya leo, kama wewe ni shabiki yangu naomba unisaidie kumwambia happy birthday ili afurahi. Mwambieni nampenda sana sana tena sana ile sanaaaaaa!!! Na namuombea kwa Mungu ampe maisha marefu.”

Ikumbukwe kwamba Mr. Blue na Waheeda walifunga ndoa Aprili 14, 2016, ikiwa ni miaka 13 tangu walipokutana kwa mara ya kwanza. Mapenzi yao yamekuwa mfano wa kuigwa katika tasnia ya burudani Nchini Tanzania.

Website |  + posts
Share This Article