Huku ugonjwa wa Mpox ukiendelea kuwa tisho kwa afya ya umma hapa nchini na kimataifa, serikali imewatahadharisha wakenya dhidi ya kula au kushughulikia wanyamapori.
Waziri wa utalii Rebecca Miano, amesema hatua hiyo inalenga kukabiliana na msambao wa Mpox, ambao umetangazwa na kituo cha kudhibiti magonjwa barani Afrika,(Africa CDC), kuwa tahadhari ya afya ya umma.
Hatua hiyo inajiri siku moja baada ya wizara ya Afya kutangaza kudhibitishwa kwa kisa cha pili cha ugonjwa huo hapa nchini, katika eneo la Malaba kaunti Busia.
Miano alisema, ugonjwa wa Mpox ni miongoni mwa magonjwa ambayo huenezwa kutoka kwa wanyama hadi kwa binadamu, na hivyo kuwataka wakenya kuwa makini hususan wale wanaoishi karibu na mbuga za wanyamapori.
Alisema wizara yake itashirikiana na shirika la huduma kwa wanyamapori KWS na washirika wengine, kuhamasisha jamii zinazoishi karibu na mbuga za wanayapori kujiepusha na ulaji wa nyama za porini pamoja na uwindaji haramu, ili kuzuia kuenea kwa Mpox.
Alitoa wito kwa wakenya kuzingatia miongozo iliyotolewa na wizara ya afya, na kuripoti visa vyovyote vinavyoshukiwa kuwa vya Mpox.