Mpango wa utoaji Afya kwa wote wazinduliwa

Tom Mathinji
2 Min Read
Uzinduzi wa mpango wa Afya kwa wote, katika uwanja wa Kericho Green.

Rais William Ruto amezindua rasmi mpango wa afya kwa wote, unaolenga kuimarisha utoaji wa huduma bora za afya ambazo ni nafuu kwa wakenya wote.

Ili kufanikisha mpango huo wa huduma nafuu za afya kwa wote, serikali imewashirikisha wahamasishaji wa aya ya jamii, ambao wataimarisha utoaji wa huduma kuanzia kiwango cha jamii.

“Jukumu kuu la wahamasishaji wa afya ya jamii, ni kutoa huduma za kuzuia maambukizi, utoaji wa elimu kuhusu afya, huduma ya kwanza kwa majeraha madogo na kuwahimiza watu kuenda hospitalini,” alisema Rais Ruto wakati wa sherehe za mashujaa katika kaunti ya Kericho.

Kulingana na kiongozi wa nchi, kila mhamasishaji wa afya ya jamii, atahudumia familia kumi katika maeneo wanakoishi.

Aidha Rais alisema hadi kufikia sasa, familia milioni moja zimetembelewa na kuhudumiwa na  wahamasishaji wa afya ya jamii, huku deta zao zikihifadhiwa katika mtandao wa dijitali wa AFYA NYUMBANI.

Siku ya Alhamisi, Rais William Ruto alisaini kuwa sheria miswada minne ya upatikanaji wa afya kwa wote.

Miswada iliyotiwa saini na Rais ni pamoja na Mswada wa Bima ya Afya kwa Jamii 2023, Mswada wa Utoaji Huduma za Msingi za Afya 2023, Mswada wa Afya ya Dijitali 2023 na Mswada wa Ufadhili wa Uboreshaji wa Vituo vya Afya 2023.

 

Share This Article