Mpango wa lishe katika shule za umma kuendelea Nairobi

Martin Mwanje
1 Min Read

Mahakama Kuu imekataa kutoa amri ya kusimamisha mpango wa lishe katika shule za umma katika kaunti ya Nairobi. 

Jaji wa mahakama hiyo Mugure Thande katika uamuzi wake amesema alizingatia maslahi bora ya mtoto kwa mujibu wa katiba.

Waziri wa Elimu wa zamani wa kaunti ya Nairobi Janet Muthoni alikuwa amewasilisha kesi mahakamani kupinga mpango huo.

Katika kesi yake, Muthoni alisema mpango huo uitwao  “Dishi na County” si halali kwani elimu inasimamiwa na serikali kuu.

Aliwasilisha kesi hiyo pamoja na shirika la kutetea haki za watoto linalojulikana kama  Tunza Mtoto Coalition Kenya.

Kupitia wakili wake Maureen Nasimiyu, Muthoni aliiambia mahakama kwamba Gavana Johnson Sakaja na Rais William Ruto hawakutia saini waraka wowote kuhamishia majukumu ya serikali kuu kwa kaunti.

Aidha, Muthoni alisema hakuna ilani yoyote ya kisheria inayoruhusu kaunti kuwalisha watoto wanaosomea shule za umma.

Kulingana na Muthoni, zaidi ya shilingi bilioni 1.7 zimetengwa na kaunti ya Nairobi kwa ajili ya mpango huo.

Kaunti ndogo anzilishi za mpango huo ni Dagoretti Kaskazini, Embakasi ya Kati, Embakasi Kusini na Kasarani.

Zingine ni Kibra, Makadara, Starehe, Roysambu, Ruaraka na Westlands.

Kaunti ya Murang’a imeanzisha mpango sawia unaowalenga wanafunzi wa shule ya chekechea.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *