Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini, IEBC imezindua rasmi mpango endelevu ulioimarishwa wa wapiga kura kote nchini, ikilenga kusajili wapiga kura wapya milioni 2.5.
Hafla rasmi ya kuzindua mpango huo ilifanyika katika kijiji cha Shimoni, eneo bunge la Lunga Lunga katika kaunti ya Kwale chini ya uongozi wa mwenyekiti wa IEBC Erastus Ethekon.

Awali, Ethekon alikuwa ameelezea kwamba tume hiyo imeajiri makarani wa usajili wapatao elfu 12 kuendesha shughuli hiyo kwa siku 30.
Ethekon alisema mpango huu mpya wa mwezi mmoja, umeundwa kwa namna ambapo utaziba mianya ambayo imekuwa ikijitokeza katika shughuli iliyokuwepo ya usajili wa wapiga kura.
Kulingana na mwenyekiti huyo, huduma za usajili wa wapiga kura zimegatuliwa chini ya mpango huo ili kuhakikisha wanafikia Wakenya wengi hasa vijana.
Wahudumu wa usajili watakuwa wakizunguka katika sehemu mbalimbali za kila wadi kulingana na ratiba ya matumizi ya mitambo ya usajili wa wapiga kura.
Watafika pia katika taasisi za elimu ya juu kama vyuo vikuu na vyuo anuwai kote nchini.
Vituo kama vile vya Huduma Centre, afisi za kuhudumia wateja za IEBC na afisi za IEBC za maeneo bunge pia vitatumiwa kusajili wapiga kura wapya.
IEBC hata hivyo imefafanua kwamba mpango uliozinduliwa leo, hautatekelezwa katika maeneo ambayo yanatarajia chaguzi ndogo hivi karibuni.