Moto wateketeza bweni la shule ya Bukhalalire, Busia

Martin Mwanje
1 Min Read

Shule ya upili ya wavulana ya Bukhalalire inayopatikana katika wadi ya Marachi ya Kati, eneo bunge la Butula katika kaunti ya Busia inakadiria hasara ya mamilioni ya pesa.

Hii ni baada ya moto usiojulikana chanzo chake kuteketeza bweni moja la shule hiyo.

Bweni hilo lilikuwa limepewa jina la Kofi Annan, kumuenzi aliyekuwa mpatanishi wa kupigiwa mfano, marehemu Kofi Annan kutoka Ghana.

Kwa mjibu wa mwalimu mkuu wa shule hiyo Mukati Didimo, moto huo ulianza wakati wanafunzi walikuwa kwenye gwaride mwendo wa saa mbili.

Lilikuwa bweni la wanafunzi 170 na hakuna yeyote aliyejeruhiwa katika mkasa huo ila kila kitu kilichokuwa ndani yake wakati huo kiliteketea.

Wakati uo huo, maafisa wa ujasusi katika kaunti ndogo ya Butula tayari wameanzisha uchunguzi wa kubaini chanzo cha moto huo.

Mwakilishi wa wadi ya Marachi ya Kati Shadrack Masinde akizungumza alipofika shuleni humo, ametoa wito kwa wanafunzi wa zamani wa shule hiyo kutoa msaada wa dharura kwa wanafunzi wa sasa.

Usimamizi wa shule hiyo umekata kauli kuwa hakuna mwanafunzi atakayerejeshwa nyumbani kufuatia mkasa huo, na kuwarai wahisani kujitokeza kutoa msaada shuleni humo.

Kisa hicho kimetokea wakati kumekuwa na visa kadhaa vya mioto iliyozuka katika shule mbalimbali nchini na baadhi kusababisha hata vifo vya wanafunzi.

Share This Article