Waziri wa biashara Moses Kuria ameomba wakenya msamaha kutokana na usemi wake katika mitandao ya kijamii.
Kuria alikuwa amechapisha taarifa kwenye mtandao wa X ambao awali ulifahamika kama Twitter akijibu lalama za wakenya baada ya bei ya mafuta kuongezeka.
Bei hiyo imezidi shilingi 200 kwa kila lita ya aina tatu kuu za mafuta kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hii.
Alisema kwamba wakenya wanastahili kujiandaa kwa bei hiyo kuongezeka hata zaidi kutokana na bei ya mafuta ghafi katika soko la ulimwengu na hali ilivyo.
Leo, Septemba 20, 2023, saa nane na dakika 21 alfajiri, waziri Kuria alitumia mtandao huo huo wa X kuomba wakenya msamaha.
“Wakenya wapendwa. Ijumaa Septemba 15, 2023, nilitoa matamshi kwamba bei ya mafuta huenda ikaongezeka hata zaidi katika muda wa miezi michache ijayo kutokana na hali ilivyo ulimwengini. Nimearifiwa na watu kama Dr Boni Khalwale na mkubwa wake kwamba maneno yangu hayakuwa sahihi, yasiyo na hisia na yenye kiburi. Nimeeleweshwa kwamba bei hiyo itashuka. Naomba radhi kwani binadamu hukosea.” aliandika waziri Kuria.
Waziri huyo amekuwa akikashifiwa sana mitandaoni kutokana na matamshi yake kuhusu suala hilo ambapo kwa mara nyingine alisikika kwenye hotuba yake akielekeza walioghadhabishwa na matamshi yake wamwonyeshe yaliko mafuta ghafi kwenye mashamba yao naye atawachimbia visima ili wayatumie.