Wenyeji Morocco walifungua makala ya 20 ya Kombe la mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17, kwa kishindo baada ya kuizabua Uganda mabao 5-0, katika mechi ya kundi A Jumapili usiku uwanjani El Bachir, mjini Mohammedia.
Ilies Belmokhtar alipachika bao kwanza dakika ya tatu, kabla ya Driss Aït Chiekh kutanua uongozi huo kwa bao la dakika ya 8.
Ziyad Baha Abedlahadj aliongeza la tatu kunako dakika ya 23, kabla ya Belmokhtar kupachika lake la pili huku wenyeji wakiongoza 4-0 kufikia mapumziko.
Morocco walihitimisha ushindi maridhawa kwa bao la tano katika dakika ya 71, kupitia kwa Ziyad Baha.
Zambia watafungua siku ya pili leo dhidi ya Tanzania katika kundi A kuanzia saa nane, kabla ya Burkina Faso kufungua mechi za kundi B dhidi ya majirani Cameroon saa kumi moja, kisha Afrika Kusini wafunge ratiba ya siku dhidi ya Misri saa nne usiku katika kundi B.
Fainali ya kipute hicho itasakatwa Aprili 19, huku timu kumi bora zikifuzu kwa Kombe la Dunia mwezi, Septemba, nchini Qatar .