Bingwa wa Dunia Mary Moraa ndiye Mkenya pekee atakayeshiriki fainali ya mbio za mita 800 katika mashindano ya Olimpiki jijini Paris nchini Ufaransa.
Moraa alifuzu kwa fainali Jumapili usiku baada ya kuongoza nusu fainali ya kwanza akiziparakasa kwa dakika 1 na sekunde 57.86.
Hata hivyo, matumaini ya Lillian Odira ambaye ni mshindi wa nishani ya fedha ya Afrika na Vivian Chebet kuingia fainali yalitumbukia nyongo.
Chebet aliburura mkia katika nusu fainali ya pili huku Odira akiridhia nafasi ya nne katika mchujo wa tatu.
Fainali ya mbio hizo itaandaliwa Jumatatu usiku huku Kenya ikiwania kutwaa dhahabu ya pili na ya kwanza tangu mwaka 2008 kupitia kwa Pamela Jelimo.