MOA kuanzisha shule ya kutoa mafunzo kwa madereva

Martin Mwanje
2 Min Read

Wamiliki wa matatu wanapanga kuanzisha shule yao ya kutoa mafunzo kwa madereva katika jitihada za kupunguza ajali za barabarani nchini. 

Kwa mujibu wa maafisa wa Chama cha Wamiliki wa Matatu, MOA, hatua hiyo inakusudia kupiga jeki jitihada za serikali kupunguza ajali za barabarani na kuhakikisha usalama wa wasafiri.

Wakiongozwa na mwenyekiti mpya wa MOA Albert Karagacha, maafisa wa chama hicho wanasema utoaji upya wa mafunzo uliositishwa kwa madereva wa magari ya umma ya kubeba abiria, PSVs haungefanikiwa kwa sababu washikadau hawakuhusishwa.

Mamlaka ya Uchukuzi wa Kitaifa na Usalama, NTSA ilikuwa imewataka madereva wa magari hayo kupewa mafunzo upya kabla ya mpango huo kusitishwa.

Maafisa wa MOA wanasema sekta ya matatu imeanza kujidhibiti yenyewe kwa kuanzisha taasisi ya utoaji wa mafunzo kama yanavyofanya mashirika mengine ya kitaifa.

Karagacha aliiyasema hayo wakati akiwahutubia wanahabari mjini Thika, kaunti ya Kiambu alikokutana na wamiliki wa matatu wakati timu yake ikianzisha majadiliano na wanachama wake kutoka kote nchini kufuatia changamoto zilizosababisha gharama za juu za mafuta.

Akiwa ameandamana na Afisa Mkuu Mtendaji wa MOA Patricia Mutheu na Mratibu wa Kitaifa Philip Muia, Karagacha alitoa wito kwa madereva kutahadhari wakati wakiwa barabarani wakati huu ambapo shule zimefungwa kwa likizo ya muhula wa pili.

Aidha maafisa hao walipuuzilia mbali majaribio ya serikali kudhibiti nauli ya magari yanayobeba abiria wakisema hatua hiyo iitagonga mwamba.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *