Volkano mashariki mwa Indonesia ililipuka usiku wa kuamkia leo Ijumaa na kuua watu wasiopungua 10 wakati ikitoa miale ya moto na majivu katika vijiji jirani, maafisa wamesema leo Jumatatu. Maafisa hao wameongeza tahadhari hadi kiwango cha juu zaidi.
Mlima Lewotobi Laki-Laki, volkano pacha yenye mita 1,703 inayopatikana katika kisiwa maarufu cha watalii cha Flores, ililipuka kabla usiku wa manane na kuzilazimisha mamlaka kuhamisha wanavijiji kadhaa.
Wakazi wameelezea hofu yao wakati kasoko ilipoanza kurusha miamba yenye moto kwenye makazi yao.
“Nilikuwa nimelala wakati ghafla kitanda kilipotikisika mara mbili ni kana kwamba mtu amekitikisa. Kisha nikagundua kuwa volkano ilikuwa imelipuka, kwa hivyo nilikimbia kuelekea nje,” alisema Hermanus Mite, msusi mwenye umri wa miaka 32.
Abdul Muhari, msemaji wa idara ya uzuiaji wa majanga ya nchi hiyo (BNPB) alithibitisha idadi ya vifo hivyo wakati wa mkutano na wanahabari. Alisema watu 10,295 waliathiriwa na milipuko hiyo.
Kulingana naye, hesabu ya idadi ya watu waliohamishwa ilikuwa bado inafanywa lakini akaongeza kuwa hakuna aliyeripiwa kutojulikana aliko.