Mawasiliano ya simu yamelemazwa katika sehemu za Wajir baada ya watu waliokuwa wamejihami wanaoaminika kuwa wanachama wa kundi la Alshabaab kuvamia na kuharibu kabisa mlingoti wa mawasiliano.
Kulingana na maafisa wa polisi, mlingoti huo muhimu wa mawasiliano wa eneo la Dasheg uliharibiwa jana Jumatano.
Wakazi waliozungumza na wanahabari leo walielezea kwamba walisikia milipuko na milio ya risasi karibu na mlingoti huo jana na leo asubuhi wakapata kwamba uliharibiwa.
Polisi wanasema polisi wa akiba waliokuwa wakilinda mlingoti huo hawakuumia kwenye shambulizi hilo la jana ila waliondoka ili kuhakikisha usalam wao.
Uchunguzi umeanzishwa huku polisi wakiunda kikosi cha kusaka wahusika wa shambulizi hilo ambalo limesababisha hali ya wasiwasi.
Kuna hofu ya mashambulizi ya wanamgambo wa Al Shabaab kurejea katika eneo hilo ambalo limeshuhudia amani na utulivu kwa muda.