Baadhi ya wazee wa eneo la Mlima Kenya Mashariki, wameelezea kuunga mkono uwaniaji Urais wa William Ruto na Kithure Kindiki, wakitoa wito wa umoja katika eneo lote le Mlima Kenya.
Waliyatangaza hayo kwenye mkutano uliowaleta pamoja wazee kutoka kaunti za Embu, Meru na Tharaka Nithi, Jumamosi asubuhi.
Huku wakitoa wito wa umoja katika eneo hilo, wazee hao walisema watajizatiti kuhakikisha watu wa Mlima Kenya Mashariki na wenzao wa Magharibi wanazungumza kwa sauti moja katika maswala ya maslahi ya pamoja, kwa kuheshimu utamaduni na taasisi za kila jamii.
“Tunatoa wito kwa ndugu na dada zetu katika eneo la Mlima Kenya Magharibi na wale walio ughaibuni, kumuunga mkono Naibu Rais Kithure Kindiki jinsi wenzao wa Mlima Kenya Mashariki wamekuwa wakiunga mkono viongozi kutoka eneo lao,” walisema wazee hao.
Walielezea imani yao kwa Prof. Kindiki kuwahudumia Wakenya, katika wadhifa wa Naibu Rais.
Wakati huo huo, walimuidhinisha Kindiki kuwa msemaji wa jamii hizo na ndiye atakayezungumza kwa niaba yao.
“Kiongozi yeyote, mtu binafsi au jamii anayetaka kuzungumza na watu wa Mlima Kenya, wakiwemo wanasiasa, atafanya hivyo kupitia Naibu Rais Kithure Kindiki,” walisema wazee hao.