Mahakama moja ya Mombasa imemhukumu kifungo cha miaka 40 mlanguzi wa mihadarati, aliyekamatwa akiwa na dawa za kulevya za thamani ya shilingi milioni 275.
Fatuma Ahmed Ali, pia alitozwa faini ya shilingi 825,642,000 katika hukumu iliyotayarishwa na hakimu mwandamizi Martin Rabera na kusomwa na hakimu mkuu mkaazi David Odhiambo.
Fatuma aliyeshtakiwa pamoja na washukiwa wengine wawili ambao hawakuwa mahakamani, alikabiliwa na makosa ya ulanguzi wa gramu 91,738 za Heroin zenye thamani ya shilingi milioni 275.
Upande wa mashtaka ukiongozwa na Barbara Sombo, ulipinga ombi la mshtakiwa la kutaka ahudumie kifungo cha nje.
Akisoma hukumu hiyo, hakimu Rabera alidokeza kuwa upande wa mashtaka uliwasilisha ushahidi wa kutosha, ikiwa ni pamoja na taarifa za maafisa ambao walifanya msako katika makazi ya mshtakiwa.
“Makosa dhidi ya mshtakiwa yamethibitishwa kikamilifu. Mshukiwa amepatikana na makosa,” alisema hakimu Rabera.
Fatuma alikamatwa Septemba 20, 2018 katika mtaa wa Kikambala Housing, kaunti ya Kilifi.