Afisa mwandamizi wa Urusi Sergei Shoigu leo Jumanne amemwambia Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi kuwa jukumu la dharura zaidi la nchi zao linapaswa kuwa kukabiliana na “uzuiaji” wa Marekani. Shoigu aliyasema hayo alipokutana na Wang kwa mazungumzo ya usalama jijini Beijing.
Urusi na China zimepanua ushirikiano wa kijeshi na ulinzi tangu Urusi ilipoamrisha vikosi vyake kuivamia Ukraine takriban miaka mitatu iliyopita. Rais wa China Xi Jinping ni mmoja kati ya washirika muhimu zaidi wa Rais wa Urusi Vladimir Putin katika jukwaa la kimataifa.
Lakini China pia imejipata katika njia panda kufuatia ushirikiano unaoongezeka kati ya Urusi na Korea Kaskazini. Kiasi kwamba Korea Kaskazini imetuma wanajeshi wake nchini Ukraine kusaidia uvamizi unaoendelea wa Urusi wa nchi hiyo.
Akizungumza na Wang jijini Beijing, Shoigu ambaye ni Katibu wa Baraza la Usalama la Urusi alisisitiza umuhimu wa China na Urusi “kukabiliana na sera ya ‘uzuiaji mara mbili’ ambayo Marekani na washirika wake wameelekezea nchi za Urusi na China”.
“Ushirikiano wa kina na kimkakati (kati ya China na Urusi) unawakilisha aina ya ushirikiano kati ya nchi mbili zenye nguvu zaidi katika dunia ya leo,” Shoigu alimwambia Wang ambaye ni mwanadiplomasia wa ngazi za juu wa China.
Kabla ya mazungumzo hayo, China ilisema maafisa hao wawili watajadiliana “masuala makuu yanayohusisha maslahi ya usalama wa kimkakati na kuboresha uaminifu wa pande mbili”.
Shoigu alikuwa Waziri wa Ulinzi wa Urusi katika kipindi cha miaka miwili ya uvamizi wa Ukraine kabla ya kuhamishiwa katika Baraza la Usalama na Rais Putin.