Mkutano wa Gavana wa kaunti ya Kiambu Kimani Wamatangi wa kusambaza hundi za ufadhili wa masomo almaarufu Bursary katika eneo bunge la Ruiru uligeuka vurugu.
Maafisa wa polisi hata hivyo waliingilia kati na kutuliza hali katika ukumbi wa kanisa la PCEA Membley wadi ya Gitothua.
Tatizo lilianza pale ambapo kundi la watu waliokuwa na ghadhabu liliingia kwenye ukumbi huo na kutaka kujumuishwa kwenye orodha ya wanaonufaika na ufadhili wa masomo.
Kwa wakati mmoja ilikuwa vigumu kusimamia umati wa watu wapatao 2000 ambao walikuwa wanataka kumzuia gavana asiondoke eneo hilo kwa kufunga lango na kugonga gari lake kwa mikono.
Wawakilishi wadi waliokuwa wakihudhuria hafla hiyo walikuwa tayari wameonyesha kutoridhika na namna Gavana alikuwa ametekeleza usambazaji wa msaada huo wa masomo wakimlaumu kwa kufanya mambo peke yake bila kuhusisha viongozi wengine.
Viongozi hao John Kamande ‘Coaches’ wa wadi ya Gitothua, Kimani wa Nduta wa wadi ya Biashara na Kennedy Odhiambo wa wadi ya Kahawa Sukari walimzomea gavana Wamatangi kwa kile walichokitaja kuwa hatua yake ya kutumia raslimali za kaunti kama chombo cha kampeni.
Wanamlaumu gavana kwa kushindwa kutekeleza ahadi alizotoa kwa wananchi wakati wa kampeni na hatua ya kurejesha kwa hazina kuu shilingi bilioni 3 za mwaka wa matumizi wa 2022/2023.
Gavana Wamatangi hata hivyo anasisitiza kwamba amejitolea kuhudumia wakazi wa kaunti ya Kiambu na hana muda na wanaompinga.
Seneta wa kaunti hiyo ya Kiambu Karungo Wa Thang’wa amehimiza wawakilishi wadi kuendelea kutekeleza jukumu lao na uangalizi wa serikali ya kaunti akisema gavana Wamatangi amekuwa akifanya kazi peke yake.
Alisema pia kwamba serikali ya Wamatangi haijakamilika suala ambalo ni kinyume cha sheria.
Mwaka mmoja tangu kuchaguliwa, Gavana Wamatangi hajaajiri katibu wa kaunti, wanachama wa kamati kuu ya kaunti katika idara fulani fulani pamoja na maafisa wakuu.
Thang’wa anasema alikuwa amempatia gavana Wamatangi muda wa mwaka mmoja arekebishe mambo lakini hawezi kusalia kimya anapoendesha kaunti kwa njia isiyofaa.
Uhusiano kati ya Wamatangi, wawakilishi wadi na viongozi wengine waliochaguliwa wa kaunti ya Kiambu umekuwa ukizorota kiasi cha Naibu Rais Rigathi Gachagua kuingilia kati.
Alifanya mkutano na wabunge wa maeneo bunge yaliyo kwenye kaunti ya Kiambu mwezi Mei kwa nia ya kusuluhisha matatizo yaliyopo lakini Thang’wa anasema hakuna lolote limebadilika.
Rais William Ruto anasemekana kumzomea Wamatangi kwa kile alichokitaja kuwa kutoelewa fika manifesto ya serikali ya Kenya Kwanza.