Rais William Ruto leo Ijumaa ameongoza mkutano wa ngazi za juu wa kongamano la ushauri kuhusu viwanda visivyochafua mazingira barani Afrika, katika Ikulu ya Nairobi.
Taarifa kutoka Ikulu inasema lengo la mkutano huo ni kuzileta pamoja taasisi kuu za kifedha barani Afrika, ili kubuni utaratibu wa kufadhili ujenzi wa viwanda visivyochafua mazingira.
Mpango huo ni juhudi za bara la Afrika mstari wa mbele katika viwanda visivyochafua mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya anga.
Mkutano huo umeandaliwa kwa ushirikiano na shirika la biashara huru barani Afrika na utahudhuriwa na wawakilishi wa taasisi kuu za kifedha barani Afrika ikiwemo tume ya muungano wa Afrika.
Kongamano hilo lililoidhinishwa na muungano wa Afrika mwezi februari mwaka huu linaangazia malengo ya Afrika ya marekebisho ya uchumi na unazingatia ahadi zilizotolewa chini ya azimio la Nairobi kuhusu mabadiliko ya hali ya anga ambayo yanatambua viwanda kuwa muhimu katika kukabiliana na mabadiliko ya hali ya anga, kutoa nafasi za kazi na kuleta maendeleo.