Mkurupuko wa kunguni Paris

Marion Bosire
1 Min Read

Jiji la Paris nchini Ufaransa limekumbwa na mkurupuko usio wa kawaida miezi michache kabla ya kuandaa fainali za michezo ya Olimpiki mwaka 2024.

Inaripotiwa kwamba kunguni wamevamia jiji hilo kwa wingi.

Wadudu hao wadogo ambao huuma na kufyonza damu wameonekana kwenye maeneo tofauti ya umma kama magari ya uchukuzi almaarufu Metro, hoteli, kumbi za maonyesho ya filamu na uwanja wa ndege wa Charles De Gaulle.

Naibu Meya wa jiji la Paris Emmanuel Gregoire alisema kupitia mtandao wa X kwamba hakuna aliyesaazwa na wadudu hao.

Alisema juhudi za pamoja zinahitajika kati ya wahudumu wa afya, jamii na wadau husika katika kutatua suala hilo haraka.

Wakazi wa jiji hilo kuu la Ufaransa waliohojiwa na wanahabari walisema waligundua alama za kuumwa na wadudu hao.

Kampuni za huduma za kuangamiza wadudu nyumbani, huduma ambayo hugharimu hadi Dola 500,  zimeripoti kwamba katika siku za hivi maajuzi wateja wameongezeka kwa sababu ya mkurupuko huo wa kunguni.

Wakazi wa mji huo wamehimizwa kusalia watulivu mipango inapotekelezwa ya kuangamiza kunguni hao.

Share This Article