Mkurugenzi wa kampuni iitwayo Vasco Real Estate Leah Muthoni Mwaura alikamatwa na kufikishwa mahakamani kutokana na kesi inayohusu ulaghai wa ardhi.
Baada ya kukwepa kukamatwa kwa muda mrefu na maafisa wa upelelezi wa jinai, DCI, Muthoni alipatwa kwenye maficho yake na alifikishwa katika mahakama ya Thika leo Jumatano.
Akizungumza mbele ya Hakimu Mkuu wa mahakama ya Thika Yusuf Baraza, Muthoni alikanusha mashtaka dhidi yake ambayo ni kujipatia pesa kwa njia ya uongo kinyume cha sehemu ya 313 ya kanuni za adhabu.
Muthoni atasalia kwenye seli za polisi kwa muda wa wiki mbili huku uchunguzi ukiendelea kuhusu kesi hiyo.
Kulingana na stakabadhi za mahakama, Muthoni anadaiwa kupata pesa kwa njia ya ulaghai mwaka 2023 kutoka kwa watu wawili alioahidi kuuzia mashamba, yeye pamoja na wengine ambao hawakuwepo mahakamani.
Alipokea shilingi milioni 8.8 kutoka kwa Richard Kimani na milioni 1.07 kutoka kwa Joseph Kinyanjui baada ya kuwahadaa kwamba angewauzia vipande vya ardhi katika eneo la Makongeni huko Thika.
Hakimu Baraza aliagiza kwamba Muthoni azuiliwe katika seli za polisi hadi Machi 3, 2025, siku ambayo kesi hiyo itatajwa ili kuunganisha mashtaka na kutathmini iwapo ataachiliwa kwa dhamana.