Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Renson Ingonga amekata rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu wa kumwondolea mashtaka Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya.
Gavana huyo alikuwa anakabiliwa na mashtaka ya utumizi mbaya wa fedha za umma na mgongano wa maslahi.
Rufaa hiyo inafuatia uamuzi uliotolewa Machi 4, 2026 na Jaji Bahati Mwamuye, uliomzuia Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP), Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI, na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kumchunguza, kupendekeza mashtaka au kuanzisha kesi ya uhalifu dhidi ya Gavana Natembeya.
Aidha, mahakama hiyo pia iliagiza kuwa Gavana huyo alipwe fidia ya shilingi milioni 2.5.
Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma alikuwa amemfungulia Natembeya mashtaka ya unyakuzi wa mali ya umma ya thamani ya shilingi milioni 3,252,568 .
Mashtaka hayo yalitokana na malipo yaliotolewa na serikali ya kaunti ya Trans Nzoia kwa kampuni zilizofanya biashara na kaunti hiyo.
Inadaiwa kuwa kati ya Januari 1, 2023 na Aprili 30 2025, Gavana Natembeya alipata fedha hizo kinyume cha sheria kwa kutumia kampuni za Lyma Agro Science Limited, Maira Stores, na Easterly Winds Limited, hatua iliyohusisha mgongano wa maslahi.