Renson Mulele Ingonga ameapishwa kama Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Mashtaka ya Umma ambapo atahudumu kwa muda wa miaka minane.
Hafla ya kumuapisha iliandaliwa leo asubuhi katika Ikulu ya Nairobi na kuongozwa na Rais William Ruto.
Haya yanajiri baada ya bunge kuidhinisha uteuzi wake kwa kauli moja na anachukua mahali pa Noordin Haji ambaye aliteuliwa na Rais kuongoza kitengo cha ujasusi nchini.
Wakati wa usaili wake bungeni, Mulele alisema utajiri wake ni wa kiwango cha shilingi milioni 300 ambazo ni nyumba na shamba ya familia.
Yeye ni wakili wa mahakama kuu na amekuwa akihudumu kama Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Mashtaka ya Umma katika eneo la Kaskazini mashariki.
Watu 15 walihojiwa na tume ya utumishi wa umma kwa wadhifa huo lakini Mulele akawapiku wote.
Rais Ruto aliahidi kumuunga mkono mkurugenzi huyo mpya wa mashtaka ya umma ili kuhakikisha haki inatekelezwa nchini.
Viongozi wengine walioshihudia uapisho huo ni pamoja na Naibu Rais Rigathi Gachagua, Waziri aliye na Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi, Jaji Mkuu Martha Koome, Spika wa bunge la Taifa Moses Wetang’ula, Mwanasheria Mkuu Justin Muturi na Waziri wa Mambo ya Ndani Kithure Kindiki.