Mke wa mfanyabiashara wa asili ya India aliyeuawa Jayesh Kumar kwa jina Velji Jayaben Jayesh kumar amekiri kwamba alitaka tu mume wake aadhibiwe na wala sio kuuawa.
Alisema hayo katika mahakama ya kibera alikopelekwa baada ya kukamatwa na sasa atasalia katika korokoro za polisi kwa siki 14 huku uchunguzi zaidi ukitekelezwa.
Kukamatwa kwa Jayaben Jumatano kulijiri baada ya uchunguzi kubainisha kwamba alikuwa akiwasiliana na mmoja wa washukiwa wa mauaji ya mume wake siku ambayo aliuawa na mwili wake kumwagiwa tindikali.
Inaaminika wanandoa hao walikuwa wakizozana na mke akaamua kutafuta huduma za rafiki katika kuadhibu mume.
Jayaben ambaye alifikishwa mbele ya hakimu Irene Kahuya hata hivyo hakuhukumiwa baada ya upande wa mashtaka kuomba azuiliwe kwa siku 21 ili wakamilishe uchunguzi lakini wakapatiwa siku 14.
Hakimu Kahuya alisema kwamba uchunguzi wa simu za washukiwa wa kesi hiyo ulibaini kwamba Velji aliwasiliana na mmoja wa washukiwa wanne akimtaka amsaidie kuadhibu mume wake.
Baadaye mshukiwa huyo alimfahamaisha Velji kwamba walikuwa wamekamilisha shughuli lakini Velji hakufurahia kwa sababu maagizo aliyotoa ni ya adhabu tu na wala sio kuua.
Uchunguzi wa DNA kwa mifupa iliyookotwa kutoka eneo la tukio bado haujafanywa kubaini iwapo ni ya Jayesh Kumar.
Jayesh Kumar aliuawa na mwili wake kuchomwa kwa kemikali katika eneo la Lukenya, kaunti ya Machakos Februari 14, 2024.