Mkataba waafikiwa kuruhusu Jamii zilizo karibu na msitu wa Mau kuutunza

Marion Bosire
2 Min Read

Jamii zinazoishi karibu na msitu wa Mau katika kaunti za Narok na Bomet zimetia saini mkataba wa miaka mitano na huduma ya misitu nchini KFS ambao utawaruhusu kutunza msitu huo huku wakifaidi kutokana na raslimali zake.

Miungano minne ya kijamii ya kutunza msitu huo ya Nyangores, Olenguruone, Olpusimoru na Nairotia ilitia saini mpango wa ushiriki wa utunzaji wa msitu ambao utawasaidia kuchangia katika utunzaji wa vyanzo muhimu vya maji.

Hafla ya kutia saini mkataba huo iliongoza na naibu mtunzaji mkuu wa misitu nchini Beatrice Mbula ambaye alisema kwamba mifumo ya usimamizi inatoa fursa nzuri inayokubalika kisheria ya jamii zinazoishi karibu na misitu kufaidi huku wakiitunza.

Alishukuru hazina ya ulimwengu ya mazingira WWF kwa kushirikiana na KFS pamoja na jamii kuanzisha mpango huo utakaodumu hadi mwaka 2027.

Alipongeza wakazi kwa upanzi wa miche ya miti akisema miche ipatayo elfu 225,imepandwa huko Narok wiki hii.

Meneja wa miradi katika hazina ya WWF Kevin Gichagi alisema hazina hiyo iliwezesha kubuniwa kwa mkataba huo na vyama hivyo vinne vywa kijamii ili kuleta uwiiano kati ya watendakazi wa huduma ya misitu na jamii zinazoishi karibu na msitu wa Mau.

Alisema WWF itaendelea kushiriki ufadhili wa utekelezaji wa mkataba uliotiwa saini ili kuhakikisha msitu uko sawa na jamii hizo zinajimudu.

Naibu kamishna wa kaunti ya Bomet Rehema Kitito alisema kwamba watunzaji misitu wa KFS walioajiriwa na serikali wamekuwa wakilinda msitu huo usiharibiwe na juhudi zao zimezaa matunda kwani hata miili iliyokuwa ikipatikana humo ya watu waliouawa sasa haipatikani humo.

Hafla hiyo iliandaliwa katika kituo cha misitu cha Masese na kuhudhuriwa na mtunzaji mazingira wa Narok Daniel Mkung, mwakilishi wa wadi ya Singorwet Josphat Kipkirui na wengine.

Share This Article