Mvua kubwa ambayo inashuhudiwa katika sehemu nyingi nchini imesababisha madhara katika mji wa Maua, eneo bunge la Igembe Kusini kaunti ya Meru.
Mji huo ambao umezungukwa na vilima umefurika.
Wakazi wa mji huo sasa wanadai kwamba mipangilio ya mji huo haikutekelezwa kwa njia ifaayo na kwamba mitaro ya kuondoa maji taka imeziba hali ambayo inasababisha maji ya mvua kujaa hadi kwenye maduka na nyumba za makazi.
Wakazi hao wanasema wanakadiria hasara kwa sababu mali zao zimeharibiwa na maji hayo ya mvua na wengi wao wameanza kuhamia miji iliyo karibu.
Sasa wanaitaka serikali kuu na serikali ya kaunti ya Meru ziwasaidie kwa mahitaji msingi kama vile chakula na malazi.
Wanataka idara husika pia katika serikali ya kitaifa na serikali ya kaunti kutathmini upya mipangilio ya mji huo ili kuepusha majanga kama vile mafuriko.