Mjadala kuhusu kuondolewa afisini kwa waziri wa kilimo na ufugaji Mithika Linturi unaendelea katika bunge la taifa. Hii ni baada ya spika wa bunge hilo Moses Wetangula kuuidhinisha juzi.
Mbunge wa Bumula Jack Wamboka ndiye mwanzilishi wa mjadala huo na katika kuuidhinisha, Wetangula alisema kwamba mbunge huyo alitimiza mahitaji yote ya kikatiba na sheria za bunge katika kuweka hoja hiyo bungeni.
Wabunge wana muda wa siku saba kujadili waziri Linturi na kuamua hatima yake.
Suala hili linatokana na usambazaji wa mbolea gushi kwa wakulima chini ya mpango wa serikali wa ruzuku ya mbolea nchini kwa lengo la kupiga jeki uzalishaji wa chakula.
Wamboka anataka Linturi aondolewe afisini kwa sababu tatu ambazo ni ukiukaji wa katiba, ukiukaji wa kifungu nambari 46 cha katiba na ukiukaji wa maadili.
Wakati wa kufungua mjadala huo leo, Spika Wetangula alielekeza kwamba wabunge wapate muda wa saa tatu kutoa maoni yao hadi saa saba mchana na baadaye mchana atatoa fursa kwa wabunge kupiga kura ya kuunga au kupinga mjadala huo.
Wamboka katika mawasilisho yake ya kuunga mkono mjadala wake alisema anahisi kwamba waziri Linturi alikosa kuwajibika ipasavyo ili kukinga wakulima kutokana na mbolea hiyo gushi.
Kulingana naye Linturi alitekeleza uhalifu na anastahili kukamatwa na kufunguliwa mashtaka.
Katika mawasilisho yake kuhusu mjadala wa kuondolewa kwa waziri wa kilimo, kiongozi wa walio wachache bungeni Opiyo Wandayi alisema kwamba suala la uwepo wa chakula linagusa ulinzi wa taifa na yeyote anayepatikana na hatia ya kuhujumu uzalishaji wa chakula anastahili kuchukuliwa hatua kali.
Kulingana na Wandayi katika nchi nyingine ulimwenguni mkosaji kama huyo huwa anahukumiwa kifo.
Mbunge mteule wa ODM John Mbadi naye alisema kwamba suala hilo sio la kupuuzwa kwani ukosefu wa chakula unaweza kutumbukiza nchi katika matatizo.
Kiongozi wa wengi bungeni Kimani Ichung’wa alimtetea Linturi akisema kwamba Wamboka katika mawasilisho yake hajadhihirisha kuhusika kwa waziri Linturi katika mchakato mzima wa manunuzi na usambazaji wa mbolea gushi kwa hivyo hana hatia.