Mivutano katika chama cha ODM imeendelea kurindima leo Ijumaa huku mirengo miwili ya chama hicho ikiandaa mikutano miwili tofauti.
Huku mrengo unaoongozwa na Dkt. Oburu Oginga ukiandaa Mkutano Maalum wa Wajumbe (SDC) katika uwanja wa Jamhuri jijini Nairobi, ule unaoongozwa na Katibu Mkuu Edwin Sifuna unaandaa Mkutano wa Kitaifa wa Wajumbe (NDC) katika ukumbi wa Ufungamano.
Tofauti kati ya pande hizo zikidhihirika kwa majina zinazotumia, mrengo wa Oburu ukijiita Linda Ground huku ule wa Sifuna ukijiita Linda Mwananchi.
Tofauti hizo zimetokota tangu kufariki kwa kinara wa zamani wa chama hicho, hayati Raila Odinga.
Kiini cha tofauti hizo ni ikiwa ODM inapaswa kushirikiana na chama tawala cha UDA kuelekea uchaguzi wa mwaka 2027.
Mrengo wa Linda Ground unamezea mate ndoa kati ya ODM na UDA wakati mrengo wa Linda Mwananchi ukipinga vikali ndoa hiyo.
Ilivyo kwa sasa, chama cha ODM kinaelekea kugawanyika rasmi mara mbili kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 huku migawanyiko kati ya mirengo hiyo ikikosa kuonyesha dalili za kufikia kikomo.