Mamia ya waombolezaji wamejitokeza leo katika ukumbi wa uwanja wa kimataifa wa Kasarani kutoa heshima za mwisho kwa marehemu mchezaji wa Voliboli Janet Wanja.
Wanja alifariki usiku wa Disemba 26 akiwa na umri wa miaka 40, baada ya kuugua saratani kwa muda mrefu.
Ibada ya maombi iliongozwa na kanisa la CHRISCO.
Huzuni na majonzi vilitanda wakati wa kuwasilishwa kwa jeneza la mwili wake katika ukumbi wa Kasarani, wengi wakishindwa kujistahimili kutokana na kumbukumbu zao kwa marehemu, wakiwemo wachezaji aliocheza nao na wale waliongia mchezoni baada yake, waliomlimbikizia sifa sufufu.
Janet Wanja Mungai alizaliwa Februari 24 mwaka 1984 katika kaunti ya Nairobi na alianza masomo katika shule ya msingi ya Kenyatta, alikofanya mtihani wa darasa la nane mwaka 1998 na kujiunga na shule ya Sacred Heart Mukumu Girls, alikohitimu kidato cha nne mwaka 2004.
Baada ya kumaliza masomo ya kidato cha nne, Wanja alijiunga na klabu ya Kenya Pipeline na KCB alikocheza kwa zaidi ya mwongo mmoja.
Mwaka 2004, aliteuliwa kujiunga na timu ya taifa kwa mara ya kwanza akishiriki Olimpiki mjini Athens, Ugiriki, akiwa na umri wa miaka 20.
Kwa jumla, marehemu alishinda mataji matano ya bara Afrika akiwa na Malkia Strikers na pia kuiwakilisha Kenya katika mashindano ya dunia, mashindano ya kombe la dunia, na mashindano ya dunia ya Grand Prix.
Katika klabu, marehemu Wanja aliichezea Kenya Commercial Bank, Kenya Pipiline na Rwanda Patriotic Army, APR na pia klabu ya Al Shabaab katika Umoja wa Milki za Kiarabu, UAE kabla ya kustaafu rasmi mwaka 2020.
Hadi kifo chake, Wanja alikuwa katika benchi ya kiufundi ya timu ya taifa ya Kenya na alikuwa nayo wakati wa michezo ya Olimpiki ya Paris, Ufaransa mwaka jana.
Kwa kawaida alikuwa mchangamfu,mcheshi na mwenye bashasha kila wakati.
Wanja alikuwa na ndugu watano: Simon Kiruthi, marehemu Julius Muritu, mchezaji soka Kevin Kimani, Linda Gachambi, na Esther Muthoni.
Misa hiyo ilihudhuriwa na viongozi kadhaa wa mashirikisho ya michezo nchini wakiongozwa na Rais wa Shirikisho la Voliboli nchini, Charles Nyaberi.
Marehemu atazikwa kesho katika makaburi ya Lang’ata.
Buriani kwa Wanja na makiwa kwa familia yake.