Serikali inakamilisha mipango ya kutoa fedha za advansi kwa wakulima wa kahawa nchini.
Naibu Rais Rigathi Gachagua anasema serikali ilikuwa imetenga shilingi bilioni 4 kwa hazina ya kahawa mbali na shilingi bilioni 2.7 zilizokuwa zimetengwa awali, ikiahidi kuhakikisha wakulima wanaostahiki wanafaidi na fedha hizo.
Aliongeza kuwa mpango huo unaboreshwa kuhakikisha utendakazi bora na uwazi.
Gachagua aliyasema hayo leo Jumanne wakati wa mkutano wa mashauriano uliofanyika katika makazi rasmi mtaani Karen na kuwaleta pamoja Waziri wa Vyama vya Ushirika Simon Chelugui na washikadau wakuu katika sekta ya kahawa.
Kulingana na Gachagua, utawala wa Rais Ruto bado unakusudia kufufua sekta ya kahawa, na kuahidi kuendelea kusimama imara dhidi ya majaribio ya kukwamisha mageuzi katika sekta hiyo.
“Hatuna shida yoyote na mtu yeyote. Shida pekee ni kuhakikisha wakulima wanapata mapato yanayostahili kwa sababu wamekandamizwa kwa muda mrefu,” alisema Gachagua.
Rais Ruto amemtwika Naibu Rais jukumu la kuongoza mageuzi katika sekta ya kahawa na pia katika sekta za kahawa na maziwa huku serikali ikilenga kuongeza uzalishaji na mapato ya wakulima.
Waziri Chelugui aliahidi kuhakikisha wakulima wanaostahiki wananufaika na hazina ya kahawa.