Miito ya Marekani kusitisha ufadhili kwa Israel imerejelewa tena kufuatia shambulizi baya katika shule moja katika ukanda wa Gaza.
Ufadhili huo unajumuisha wa kifedha pamoja na wa silaha ambao watetezi wa haki za binadamu wanasema unachangia pakubwa dhuluma dhidi ya watu wa eneo hilo.
Kulingana na shirika la ulinzi la Gaza wapalestina wapatao 100 waliuawa huku wengine wengi wakiachwa na majeraha katika shambulizi hilo la Jumamosi katika shule ya Al-Tabin jijini Gaza.
James Zogby mmoja wa waanzilishi wa taasisi ya Uarabuni na Marekani ambaye pia ni Rais wa taasisi hiyo anasema kwamba Marekani na wandani wake wanasema vita vitashitishwa karibuni lakini waonacho wapalestina ni vifo zaidi, kupoteza makazi na matumaini.
Ametaja kinachoendelea kuwa mauaji ya halaiki akisema muda wa kumaliza hali hiyo umeshapita lakini Israel haitaki amani au kukomeshwa kwa vita kwani bado inapokea silaha.
Inaripotiwa kwamba bomu ndogo iliyoundwa nchini Marekani aina ya “GBU-39” ndiyo ilitumika katika shambulizi la shule ya Al-Tabin.
Shambulizi hilo limetekelezwa wakati Rais wa Marekani Joe Biden anaendelea kupokea shinikizo za kukomesha usambazaji wa silaha kwa Israel huku mashambulizi ya nchi hiyo katika ukanda wa Gaza yakiwa yamesababisha vifo elfu 39,700 kufikia sasa.
Mashirika kadhaa ya kutetea haki za binadamu yametaja hatua ya Israel ya kutumia silaha za Marekani kuwa ukiukaji wa sheria ya kimataifa kuhusu haki za binadamu hali isiyoambatana na sheria za Marekani.
Lakini msemaji wa wizara ya mambo ya nje nchini Marekani alitangaza Ijumaa kwamba Marekani itatoa ufadhili wa dola bilioni 3.5 kwa Israel itakazotumia kununua silaha na vifaa vingine vya kivita vilivyoundiwa nchini Marekani.