Miili ya wanandoa yapatikana ikioza chumbani Makueni

Marion Bosire
1 Min Read

Polisi mjini Wote kaunti ya Makueni, wanachunguza kisa ambapo miili miwili mmoja wa mwanamke na mwingine wa mwanaume, iliyokuwa ikioza imepatikana kwenye nyumba moja ya kukodisha mtaani Bangladesh.

Majirani wanasema waligundua kuhusu vifo vya wawili hao kutokana na uvundo uliokuwa unatoka kwenye nyumba ambayo mwanamke huyo alikuwa amekodisha.

Mwanaume naye alikuwa na chumba chake kando ingawa wanafahamika kuwa wapenzi.

Baada ya kukosa kumwona kwa siku nne na uvundo mkali kutoka kwenye chumba chake majirani walishuku ndiposa wakafahamisha maafisa wa polisi.

Polisi walifika kwenye chumba hicho wakapata mwili wa mwanamke huyo ukiwa kifudifudi kwenye kiti na majeraha ya kisu huku mwili wa mwanaume ukiwa umening’inia kutoka kwenye paa la Nyumba hiyo.

Jackyline Mwende ambaye ni jirani yao alisema kwamba aliona wawili hao mwishi Jumamosi wakati walikuwa wakizozana usemi uliokaririwa na mlinzi wa nyumba hizo za kukodisha Paul Mutisya Mutua.

Majirani wanasema walizoea kuona na kusikia wapenzi hao wakizozana mara kwa mara na huenda hilo ndilo lilisababisha mauti yao.

Wakazi wa eneo hilo waliohofishwa na vifo vya wawili hao wametoa wito kwa wanandoa kutafuta ushauri mizozo inapotokea.

Miili ya wawili hao ilipelekwa kwenye makafani ya hospitali ya rufaa ya Makueni.

Share This Article